ESOSHI 2

BLOG HII IMEDHAMINIWA NA ESOSHI GENERAL TRADING COMPANY LTD WAKALA WA TANGA FRESH

TANGAZO

Tuesday, January 17, 2017


MASAUNI AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA MAHAKAMA YA UMOJA WA MATAIFA (UNMICT-TAWI LA ARUSHA), JIJINI DAR ES SALAAM 
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia) akimkaribisha Mkuu wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa (UNMICT), Ofisi ya Arusha, Samwel Akorimo wakati viongozi wa Mahakama hiyo walipomtembelea kiongozi huyo wa Wizara, ofisini kwake, jijini Dar es Salaam leo, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya UNMICT na Wizara hiyo. Katikati ni Msajili wa Mahakama hiyo, Dk. Elias Olufemi.  
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa (UNMICT), Ofisi ya Arusha, Samwel Akorimo (kulia) wakati alipokuwa akifafanua jambo kuhusiana na masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya UNMICT na Wizara hiyo. Wapili kulia ni Msajili wa Mahakama hiyo, Dk. Elias Olufemi. Mazungumzo hayo yalifanyika ofisini kwa Naibu Waziri, jijini Dar es Salaam  January 17.2017. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


WAZIRI MKUU AFUNGUA DUKA LA DAWA MPANDA
*Ni la MSD litahudumia mikoa mitatu ya kanda ya Tabora
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda lilogharimu sh. milioni 55 litakalohudumia mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Tabora.
Pia duka hilo itatoa huduma kwa vituo vya kutolea huduma za afya 580 ikiwa ni pamoja na hospitali za rufaa za mikoa miwili ya Kigoma na Tabora, Hospitali za wilaya sita za Nzega, Igunga, Urambo, Kibondo, Kasulu na Mpanda Mji.
Waziri Mkuu amefungua duka hilo la dawa la MSD, lililoko  katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi leo (Jumanne, Januari 17, 2017) ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa MSD Agosti 20, 2016 alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Katavi. Aliuagiuza  uongozi MSD kujenga duka hilo ili kurahisisha upatikanaji wa dawa katika mkoa huo pamoja na mikoa jirani.
Aidha, Waziri Mkuu amesema baada ya kufunguliwa kwa duka hilo Serikali haitarajii kusikia tena katika vituo vya afya na Zahanati zilizoko mkoani Katavi na mikoa jirani  zinakosa dawa. Amewaagiza Wakurugenzi kusimamia suala hilo na kuhakikisha vituo vyote vya afya vinakuwa na dawa za kutosha.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kukutana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kutafuta namna bora ya kutumia fedha za huduma za afya zinazipatikana katika halmashauri nchini.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Katavi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Amesema lengo la Serikali ni kuwa na Hospitali ya Rufaa kwa kila mkoa, hivyo, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mipya itakayojengwa Hospitali ya Mkoa ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Laurean Bwanakunu amesema ujenzi waduka hilo la Mpanda hadi kukamilika umegharimu sh. milioni 55, huku benki ya CRDB ikitoa sh. milioni 50 na MSD imeweka dawa na vifaa tiba vya sh. milioni 104.45 na vifaa vya TEHAMA vya sh. milioni tano.
Amesema kuanzishwa kwa duka hilo kutaongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa hasa dawa ambazo hazimo katika orodha zilizoidhinishwa na Serikali kutumika katika vituo vyake vya kutolea huduma za afya ila zimeidhinishwa kutumika nchini na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Amesema dawa na vifaa tiba vilivyomo katika orodha ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zinapatikana katika duka hilo kwa bei nafuu, hivyo kuondoa usumbufu kwa wagonjwa kwenda kuzitafuta katika maduka ya mbali na kwa bei ghali.
“Nitoe mfano mdogo wa tofauti ya dawa katika ya maduka ya MSD na maduka ya mitaani, hapa dawa ya sindano ya kutibu fungus aina ya Fluconazole inauzwa sh. 2,300 na mitaani sh. 4,500 na dawa ya sindano kwa ajili ya kushusha kisukari (Insulin) chupa moja MSD ni sh. 8,500 na mitaani sh. 20,000,” amesema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17, 2017.

Thursday, January 5, 2017

WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KUMZIKA KAPTENI MHAIKI
Wakati wa kuweka shada  kwenye kaburi

Wednesday, January 4, 2017


​​
WAZIRI MKUU AKAGUA GHALA LA NFRA SONGEA
*Aagiza akiba iliyopo itunzwe hadi msimu ujao wa mavuno
* RC, Ma-DC, Ma-DED waagizwa kuelimisha umma utunzaji wa chakula

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.

Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.

“Angalieni ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka.”

“Kama mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula,” alisisitiza.

“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima lakini hadi kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani ya sh. bilioni 5.28.

Alisema kanda ya Songea ni miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.

“Kanda ya Songea inayo maghala sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka. Lakini hivi sasa kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa Hifadhi (NFRA Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.

“Kanda ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani 56,000 mradi huu utakapokamilika.”

Alisema kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 85,000 ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.

Alipoulizwa ni kwa nini hawajaweza kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma alisema kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza (kawaida ni Julai mosi kila mwaka).

“Kuimarika kwa barabara za mkoa kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo kuwawezesha wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia sokoni na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima ambao alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. “Ubora hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye nafaka zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na takataka,” alisema.

Waziri Mkuu  anatembelea wilaya ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme katika kijiji cha Mtepa, atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako pia atazungumza na watumishi wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la miti la TFS katika kijiji cha Wino.IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 5, 2017.